Nafasi ya mwingiliano fani katika kukuza fasihi ya watoto
Abstract
Katika juhudi za kusawiri uhalisia wa kijamii, fasihi aghalabu hulenga hadhira fulani kwa kutumia vigezo mbalimbali. Miongoni mwa vigezo hivyo ni kuwa kutegemea uzito wa maudhui na uchangamani wa msuko, kazi ya fasihi inaweza kufumiwa ama watu wazima au watoto. Fasihi ya watoto huwa na upekee wa kimtindo, fani na hata wa kimaudhui. Wasanii wa fasihi ya watoto aghalabu hufuma kazi zao kwa kuhulutisha fani mbalimbali kwa njia inayofanikisha ung’amuzi wa yaliyomo, uibuaji wa hisia na uzidishaji wa athari kwa watoto ambao huwa hawajakomaa kiakili. Kwa hiyo, mwingiliano fani unaohusisha picha na fani za kifasihi huwa na dhima ya kubainisha na kujaliza uelewekaji wa maudhui na kumbukizi za vitushi muhimu kwa watoto. Ni kwa mkabala huu ambapo makala haya yananuia kuaninisha jinsi vipengele vya fani vinavyotumiwa katika vitabu vya fasihi ya watoto vinavyoingiliana katika kufanikisha malengo ya waandishi. Utafiti uliofanywa kwa minajili ya kuandaa makala haya uliongozwa na Nadharia ya Umuundo iliyoasisiwa na Ferdinand De Saussure (1916). Nadharia hii inajibainisha kwa kuangalia ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu kizima. Kwa kuongozwa na nadharia hii tulichukulia fasihi kuwa kitu kizima kinachojengwa kwa maudhui na fani. Katika ngazi ya pili fani nayo imeundwa kwa vipengele mbalimbali vya lugha kama vile methali, misemo, nahau, taswira, picha na tashbihi. Vipengele hivi vilitambuliwa na matumizi yavyo yakafafanuliwa na kuelezwa. Utafiti huu uliteua kimakusudi riwaya za Kisasi Hapana, Nimefufuka, Sitaki Iwe Siri, na Wema wa Mwana katika kuchunguza jinsi mwingiliano fani unavyofanikisha kazi za fasihi zinazolenga watoto.
Collections
- School of Education [21]
The following license files are associated with this item: